Serikali ya Tanzania imeweka wazi sababu za kuwakamata na kuwarudisha makwao, wanaharakati kutoka Kenya na Uganda, waliokuwa wamefika jijini Dar es Salaam, kushuhudia kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.
Tukio hilo limeibua mjadala mkubwa kuhusu uhuru wa mahakama, uhusiano wa kikanda na nafasi ya wanaharakati katika muktadha wa haki za binadamu Afrika Mashariki.
Akizungumza na wanahabari jijini Dodoma, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro, alisema wanaharakati hao, walikamatwa kwa sababu hawakuwa na leseni za uwakili, zinazowaruhusu kushiriki katika shughuli za kisheria nchini Tanzania.
Aliongeza kuwa ujio wao, ulikuwa na nia ya kuvunja sheria za nchi.
Watu waliokumbwa na hatua hiyo, ni pamoja na mwanaharakati maarufu wa Kenya, Boniface Mwangi, na Agather Atuhaire kutoka Uganda, ambao walikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi kati, Dar es Salaam, kabla ya kuachiwa na kurejeshwa makwao.
Hali hiyo imejiri baada ya wanasiasa wengine kama Martha Karua na Jaji Mkuu Mstaafu wa Kenya, Willy Mutunga, kuzuiwa kuingia nchini, punde tu walipotua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

