WABUNGE WA PWANI WASHINIKIZA SERIKALI KUU KUKAMILISHA MIRADI MIKUBWA YA MAENDELEO UKANDA HUU.

Wabunge wa Pwani wanasema wataendelea kupigania masuala ya maendeleo eneo hili, ili kupata ufadhili wa miradi katika bajeti ya mwaka ujao.

Wakiongozwa na mwenyekiti wao Danson Mwashako, wamesema kuwa serikali ya kitaifa, inapaswa kufanikisha miradi yake ukanda huu, hatua ambayo itaboresha uchumi wa Pwani.

Akizungumza katika kikao kilicho waleta pamoja viongozi wa Pwani, katika kaunti ya Kisumu, Mwashako ambaye pia ni mbunge wa Wundanyi kaunti ya Taita Taveta, ametaja mradi wa bandari ya Lamu, kuwa kati ya ile inayopaswa kupewa kipaumbele na kukamilishwa kwa haraka.

Mwashako amesema kuwa kwa sasa taifa la Kenya, likabiliwa na uhaba wa rasilimali zinazoweza kupatia taifa hili mapato ya juu na hivyo kuna haja ya serikali ya kitaifa, kuongeza fedha zinazo tengewa maeneo eneo la Pwani, ili kukamilisha miradi iliyo kwama.