WABUNGE WATAKIWA KUSAIDIA WANANCHI WAO KUPATA VYETI VYA USAFIRI WA MATAIFA YA NJE.

Viongozi wa bunge la kitaifa nchini wametakiwa kuwasaidia vijana kutafuta stakabadhi hitajika, ili kunufaika na ajira za mataifa mengine, kupitia wizara ya leba nchini.

Ni wito ambao umetolewa na katibu katika wizara hiyo Shedrack Mwadime, ambaye amewapongeza wabunge, kwa kufadhili ujenzi wa miundo msingi na hata karo za wanafunzi wa vyuo vikuu na shule za sekondari na kuwataka sasa kuzingatia kuwasaidia vijana hao.

Mwadime amesema wengi wao, wameshindwa kupata stakabadhi hitajika ili kupata nafasi hizo za ajira, jambo ambalo limechangia wengi wao kuendelea kusalia majumbani pasi na ajira, licha yao kuwa na elimu ya hali ya juu.

Vile vile Mwadime amesisitiza viongozi wa makanisa pia, kuchukua jukumu sawia na hilo na kuwasaidia vijana kupata ajira, zitakazo wawezesha kuwa wenye manufaa katika jamii zao.