Nahodha wa kikosi cha KYISA cha kaunti ya Kilifi kwenye mchezo wa voliboli Kombe Omar anasema ipo haja ya viongozi wa serikali lakini pia jamii kwa jumla kuanza kukumbatia michezo mingine kwa mfano huo wa Volibali tofauti na mchezo uliozoeleka wa soka katika kaunti hii.
Amesema mchezo wa voliboli umemletea manufaa mengi kama kijana akihoji kuwa iwapo utapewa nafasi na kufanywa kuwa maarufu kama michezo mingine huenda vijana wengi wakazidi kunufaika.
Ni kauli ambayo inaungwa mkono na mwenyekiti wa mchezo huo katika gatuzi la Kilifi Jimmy Ngalla ambaye anahoji kuwa ipo haja sasa kuhamasisha jamii kuhusu voliboli kuanzia mashinani.
Amesema kumekuwa na changamoto ya kupata wachezaji kutokana na wazazi wao kukosa kuelewa mchezo huo pamoja na safari ndefu za kufika viwanjani, hivyo maandalizi ya kuanzisha mashindano kila eneo bunge yanaendelea.

