Baadhi ya Viongozi wa Muungano wa Kenya Kwanza na wale wa chama cha PAA kaunti ya Kilifi wameamua kuweka kando tofauti zao za kisiasa ili kuwafanyia kazi wenyeji.
Kwenye kikao na waandishi wa Habari, Viongozi hao wakiogozwa na David Kadenge ambaye alikua mwakilishi wa wadi ya Malindi Mjini kaunti ya Kilifi amesema licha ya kuwa kulikuwa na tofauti za kisiasa miongoni mwao wakati wa kipute cha uchaguzi mkuu wa Agosti 9 mwaka jana wa 2022, huu ni wakati wa kufanya kazi kwa pamoja bila kutofautiana kivyama au kimirengo.
Amesema ni kupitia umoja pekee ndipo Wenyeji wa Pwani wataendelea kutekelezewa maendeleo kutoka kwa serikali za kaunti ya ile ya Kitaifa.
Naye Moses Matano ambaye ni mkereketwa wa maswala ya siasa kaunti ya kilifi amesema kuna haja ya kuunga mkono ajenda za rais William Samoei Ruto ili kufanikisha miradi ya maendeleo katika taifa la Kenya.
Wakati huohuo viongozi hao wameikosoa mikutano inayoandaliwa na muungano wa Azimio La Umoja One Kenya hasa kupanga maandamano wakisema huu sio wakati wa kuendeleza siasa nchini bali wanapaswa kutekeleza mambo ambayo yatawanufaisha Wakenya na sio kuwagawanya.
VIONGOZI WA CHAMA CHA PAA NA WA KENYA KWANZA KAUNTI YA KILIFI WAMEAHIDI KUWEKA KANDO TOFAUTI ZAO ZA KISIASA

