Huku bunge la kaunti ya Kwale likitarajiwa kuwaapisha wajumbe wa bunge hilo kesho siku ya Jumatano, tayari baadhi ya viongozi wamewasilisha majina yao kuwania nafasi ya uspika wa bunge hilo.
Wakili Michael Ganzala ni miongoni mwa viongozi wanaomezea mate nafasi hiyo kumrithi Sammy Ruwa anayetetea wadhifa huo kwa mara ya tatu.
Akizungumza mjini Kwale, Ganzala amesema analenga kuhakikisha bunge hilo linakuwa na umoja ili kupitisha miswada kwa manufaa ya wananchi.
Wakati huohuo, wakili huyo amesema yuko tayari kufanya kazi pamoja na wawakilishi wa bunge hilo endapo watamchagua katika wadhifa huo.
Wengine wanaowania wadhifa huo ni pamoja na wakili Mwatela Kamanza, mshauri wa kisheria katika afisi ya gavana wa Kwale Salim Gombeni, mwakilishi anayeondoka wa wadi ya Dzombo Patrick Mangale na aliyekuwa mbunge wa Msambweni Omari Zonga.

