Tume ya ardhi nchini imesema kuwa itatoa taarifa kamili kuhusiana na malipo ya fidia, kwa waathiriwa wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Malindi kaunti ya Kilifi miezi miwili kuanzia sasa.
Kulingana na mwenyekiti wa tume hiyo Gershom Otachi, sharti tume hiyo ifanye uchunguzi wa uhalali wa hati miliki za ardhi hizo, ili kubaini wale wanaopaswa kulipwa fidia kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza baada ya kufanya kikao hapa mjini Malindi kaunti ya Kilifi, Otachi vile vile amesema kuwa tume hiyo, bado inapaswa kuchunguza ukweli kuhusiana na iwapo, waathiriwa hao wanapaswa kulipwa fidia ya majengo yao katika eneo hilo.
Kwa upande wao baadhi ya viongozi wa wanajamii walioathirika na mradi huo Harrison Mvoi na Festus Katana, wameitaka tume hiyo kuweka wazi mikakati yao, kuhusiana na malipo hayo, kwani wamekuwa wakihangaishwa na serikali pasi na kupata suluhu la kudumu dhidi ya utata huo.

