Kenya imenufaika na ufadhili wa shilingi bilioni 1.8, kutoka kwa taifa la Uchina, fedha zitakazo tumika kuboresha hospitali mbalimbali za umma humu nchini.
Makubaliano ya utoaji wa msaada huo, yalitiwa saini na Waziri wa Fedha humu nchini John Mbadi na Balozi wa China katika taifa hili Guo Haiyan, katika makao makuu ya afisi za Wizara ya Fedha jijini Nairobi.
Wizara ya Fedha, imetaja msaada huo kuwa muhimu mno, katika juhudi za serikali ya Kenya Kwanza, kuboresha shughuli za utoaji wa huduma katika hospitali za umma.
Baadhi ya hospitali zitakazo nufaika na msaada huo ni pamoja na ile ya rufaa ya Londiani na Baringo.
Hospitali zingine zitakazonufaika ni zile zilizoko katika kaunti ya Kilifi, Misikhu katika kaunti ya Bungoma, Bildad Kagia, kaunti ya Murang’a na Chuo cha Mafunzo ya Wakulima cha Kaimosi kaunti ya Vihigha.
Wakati wa hafla hiyo, Waziri Mbadi aliishukuru serikali ya Uchina kwa msaada wake endelevu kwa Kenya, akisisitiza kuwa ushirikiano huo unaashiria uhusiano thabiti, uliopo kati ya Kenya na China.
Msaada huo, unakuja wakati ambapo Kenya imeimarisha juhudi za kuhakikisha raia wake wote, wanapata huduma bora za afya.
Kenya inalenga kufikia lengo hilo, kupitia bima ya matibabu inayotolewa kupitia Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), iliyozinduliwa mwaka jana.