TEDDY MWAMBIRE AMEAHIDI KUSHIRIKIANA NA VIONGOZI WA KAUNTI YA KILIFI

Aliyekuwa mbunge WA Ganze kaunti ya Kilifi, Teddy Mwambire sasa ndiye spika wa bunge la kaunti ya Kilifi, baada ya kupata Kura 37 dhidi ya mpinzani wake wa karibu James Charo Lewa wa chama ca PAA, aliyepata Kura 13 kati ya 51 huku Ian Amani, akipata kura moja na wengine wakiambulia patupu bila kupata kura hata moja.

Akizungumza na wanahabari baada ya kukabidhiwa rasmi afisi ya spika pamoja na vifaa vya kazi, Mwambire ambaye pia ni katibu wa ODM kaunti ya Kilifi, amesema kuwa atashirikiana na afisi ya Gavana ili kuhakikisha kuwa, wanatekeleza majukumu yao kwa wananchi kiukamilifu.

Kwa upande wake Spika anayeondoka afisini Jimmy Kahindi, amempongeza Mwambire  huku akielezea kuwa na imani kuwa Mwambire atafanya vyema shughuli za bunge hilo, kwani aliwahi kuwa naibu wa spika katika bunge hilo na kumtaka kuhakikisha kuwa baadhi ya sheria zilizotungwa na kupitishwa katika bunge hilo zinatekelezwa na serikali ya kaunti.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Mung’aro, ambaye amesema kuwa utekelezwaji wa maendeleo katika serikali ya kaunti, unategemea pakubwa kauli za wajumbe katika bunge hilo la kaunti.