Shughuli za upasuaji wa miili iliyofukuliwa katika msitu wa Shakahola kule eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi zimeanzishwa rasmi hii leo na maafisa wa idara ya afya wakiongozwa na mwanapatholojia mkuu wa serikali Johansen Oduor.
Kulingana na waziri wa usalama wa ndani profesa Kithure Kindiki shughuli hiyo ya upasuaji wa miili takriban 109 inatarajiwa kuchukua muda usiozidi wiki moja ili kufahamu chanzo cha vifo vya wakenya hao.
Akizungumza na wanahabari katika makafani ya hospitali ya rufaa kaunti ndogo ya Malindi kaunti ya Kilifi, waziri huyo amesema kuwa huenda shughuli hiyo ikachelewa zaidi iwapo watashuhudia changamoto mbali mbali ambazo kwa sasa hawajakisia kuwa huenda zikatokea.
Kwa upande wake mwanapatholojia Johansen Oduor amesema kuwa wako tayari kutekeleza shughuli hiyo kwa ustadi ili kulifanikisha kikamilifu.

