RAIS WILLIAM RUTO AAHIDI KUTEUA MAKAMISHNA WA KUCHUNGUZA VIFO VYA SHAKAHOLA KAUNTI YA KILIFI.

Rais William Ruto amesema atateua jopo la makamishna ambao watatwikwa jukumu la kuangazia chanzo cha imani na mafunzo ya itikadi potofu, katika eneo la Shakahola eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi.

Kulingana na rais ni kuwa makamishna hao, watachunguza baadhi ya maafisa wa idara ya usalama, wanaodaiwa kuzembea katika utendakazi wao na kuruhusu mchungaji mwenye itikadi potofu Paula Mackenzie, kuendeleza mafunzo hayo.

Akizungumza katika kaunti ya Pokot Magharibi, wakati kwenye ibada ya siku ya jumapili, Rais amesema kuwa makamishna hao, pia watasaidia kuzuia tukio kama hilo katika siku za usoni humu nchini.

Kiongozi huyo wa taifa amesema  kuwa wapo baadhi ya maafisa katika idara ya usalama kaunti ya Kilifi, ambao tayari wamepewa uhamisho kutokana na tukio hilo, ili kutoa nafasi ya wao kuchunguzwa iwapo walihusika katika kuendelezwa kwa dini hiyo potofu.