SERIKALI YA KITAIFA YASISITIZWA KUTATUA CHANGAMOTO ZA UMILIKI WA ARDHI ENEO BUNGE LA MAGARINI KAUNTI YA KILIFI.

Baadhi ya viongozi wa kisiasa kaunti ya Kilifi, wamemtaka rais William Ruto kutatua changamoto za uskwota katika eneo bunge la Magarini na kaunti ya Kilifi kwa jumla.

Wakiongozwa na spika wa bunge la seneti Amason Kingi, wamesema kuwa idadi kubwa ya wakaazi wa kaunti ya Kilifi, wameendelea kuishi kama maskwota katika ardhi zao, kutokana na historia za umiliki wa ardhi.

Akizungumza katika mazishi ya babake kule Kamale eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi, Kingi amewahakikishia wananchi kuwepo kwa mikakati ya kutatua mzozo wa ADC, katika wadi hiyo ya Adu eneo bunge la Magarini.

Kwa upande wake gavana wa kaunti ya Kilifi, Gideon Maitha Mung’aro, amesema kuwa hatua ya jamii za eneo hilo la Adu kupata hati miliki, itawasaudia pakubwa kujiendeleza kiuchumi.

Naye Seneta wa kaunti ya Kilifi, Stewart Madzayo ameshikiza serikali kuu kutoa suluhu dhidi ya utata huo huku akisema kuwa, hali ya uchochole wa jamii za Kamale, umechangia pakubwa wananchi hao kudulumika katika suala la umiliki wa ardhi.