Rais William Ruto anaahidi kuwezesha michezo kuwa kitega uchumi kwa vijana wengi katika taifa hili kama njia moja ya kuwakwamua kutokana na umaskini.
Ruto ambaye alikuwa anahotubia taifa Jumatatu katika sherehe za Jamhuri alisema kwamba analenga kutumia mradi wa Talanta Hela kama njia ya kuwafanya vijana kutangaza talanta zao kutoka mashinani na kupitia mradi huo kujipatia mapato.
Ruto aliahidi kuanzishwa kwa mashindano ya soka ya Botton Up yatakayofayika katika kaunti 47, mashindano ambayo yatahusisha wachezaji wasiozidi umri wa miaka 19.
Alisema analenga kufanya kazi na kila gavana wa kaunti zote ili kukuza michezo ya mashinani hasa mchezo wa soka na fainali za mashindano hayo kufanyika kila siku ya Jamhuri.
Ruto pia aliongeza kwamba mashindano hayo yatasaidia kujenga kikosi cha taifa ambacho kitawakilisha taifa hili katika ngazi za kimataifa wanapolenga kuandaa mashindano ya afcon mwaka 2027 pamoja na kuanza kuwinda tiketi ya kucheza mashindano ya kombe la dunia 2030

