Mwakilishi wa wadi ya Adu eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi, Samsson Zia amelalamikia kutokamilika kwa ujenzi wa vituo vingi vya afya katika wadi yake na kusema inasababisha wenyeji kukosa huduma za matibabu.
Kulingana na Zia ujenzi wa kituo cha afya cha Shakahola, Adimae Adu na Chakama, ulisitishwa mwaka wa kifedha wa 2015 – 2016 na kusema kituo cha afya cha Kadzandani pia kilisitisha shughuli za kutoa huduma za afya tangu mwaka wa 2022 bila kuwepo kwa maelezo kamili.
Akizungumza katika bunge la kaunti ya Kilifi wakati akitoa ripoti kuhusiana na masuala ya afya katika wadi yake, Zia ameitaka idara ya afya kaunti ya Kilifi, kuelezea chanzo cha kusitishwa kwa shughuli za utaoji huduma hizo kwa wananchi katika eneo lake.
Wakati huohuo amelalamikia ukosefu wa madawa katika vituo vingi vya afya vilivyoko ndani ya wadi hiyo ya Adu na kusema ipo haja ya serikali ya kaunti ya Kilifi kupitia idara ya afya, kuelezea mikakati iliyopo ili kukabiliana na suala la ukosefu wa madawa katika vituo hivyo.
SAMSON ZIA ALALAMIKIA KUTOKUKAMILIKA KWA UJENZI WA VITUO VINGI VYA AFYA WADI YA ADU

