RAIS WILLIAM RUTO AWAKASHIFU WAPINZANI WAKE.

Rais William Ruto hii leo ameelekeza siasa zake katika eneo la Njukini, kwenye mpaka wa kaunti ya Taita Taveta na Kajiado wakati akielezea mikakati ya serikali, katika kuboresha shughuli za maendelo kwenye jamii.

Katika hotuba yake kwa wananchi eneo hilo, Ruto amewasuta wapinzani wake, wanaoendeleza mipango ya kushirikiana ili kufanikisha ajenda ya kumbadua mamlakani kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Ruto amewasuta viongozi wa upinzani nchini, kwa madaia ya kukosa kuwa na ajenda maalum za kuboresha maisha ya wakenya na badala yake kuwataka wananchi kujitenga na viongozi hao…

Ruto ameongeza kuwa jukumu lake kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kuwa anawaleta pamoja viongozi wote wa kisiasa nchini, pasi na kuzingatia chama ama mirengo yao na kushirikiana katika kutumikia wakenya.

Aidha, gavana wa kaunti ya Taita Taveta, Andrew Mwadime pamoja mwenzake wa Kajiado, Joseph Ole Lenku, wamepongeza uzinduzi wa barabara za eneo hilo la Njukini na miradi mingine mingi eneo la Pwani.
Vile vile Rais William Ruto ameendelea kupigia debe bima mpya ya afya ya SHA licha ya mpango huo kukabiliwa na changamoto nyingi na kuwasisitiza wakenya eneo hilo, kujitokeza na kusajiliwa kwenye mpango huo, ili kunufaika na matibabu wanapougua.
Amesema kuwa hatua ya wakenya kujisajili kwenye bima hiyo, kutasaidia serikali kufanya utafiti wa wale wasio kuwa na uwezo, ili wagharamikiwe matibabu yao na serikali kuu, pasi na kulipa fedha zozote.
Rais Ruto aidha amesema kuwa lengo kuu la serikali ya kitaifa ni kuhakikisha usawa kati ya wakenya wote, wanaotafuta huduma za matibabu kwenye hospitali zote humu nchini.