RAILA ODINGA ADAI KULIKUWA NA MITAMBO MINNE YA IEBC KUPEPERUSHA MATOKEO YA UCHAGUZI

Kinara wa Azimio La Umoja One Kenya Raila Odinga anadai kulikuwa na mitambo minne ya tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kupeperusha matokeo ya kura za uchaguzi mkuu wa Agosti 9 mwaka jana wa 2022 ambazo zilitumika kufanikisha wizi wa Kura za urais katika kipute hicho.
Akizungumza katika kaunti ya Mombasa Raila amesema mitambo hiyo ilikuwa imewekwa katika sehemu mbalimbali ili kufanikisha wizi wa kura.
Raila ambaye alikuwa akizungumza kwenye kikao na viongozi wa muungano huo kutoka kanda ya Pwani amesema baadhi ya mitambo hiyo ilikuwa katika nchi za nje kama lile la Uholanzi.
Kwa mujibu wa Raila Mitambo hiyo ilisababisha kupunguzwa kwa kura zake kwenye ngome zake za kisiasa na kuongozwa kwa Rais William Samoei Ruto ambaye alitangazwa mshindi kwenye kipute hicho cha kuwania wadhifa wa urais na pia ameikosoa kamati ambayo ilibuniwa kuteua makamishna wa IEBC akisema haina usawa.
Kwa upande wa viongozi ambao walikuwa wameandamana na Raila akiwemo gavana wa kaunti ya Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir miongoni mwa wengine wameikosoa serikali ya Kenya Kwanza kwa madai inaendelea kuwakandamiza Wananchi na wameahidi kuelekea Nairobi kwenye maandamano ya Muungano hu kuishinikiza serikali kuu kupunguza gharama ya maisha.