Magoli mawili ya Martin Odegaard na moja la Gabriel Jesus yametosha kuwapa Gunners ushindi ugani emirates usiku wa kuamkia leo.
Odegaard raia wa Norway aliwapa Arsenal uongozi wa mechi hiyo kwa kucheka na wavu dakika ya 18 kabla ya kuongeza goli la pili kunako dakika ya 31.
Dakika tatu baadae Gabriel Fernando de Jesus aliwapa Gunners goli la tatu akifanya kipindi cha kwanza kutamatika kwa magoli 3 bila jawabu faida kwa wenyeji.
Hata hivyo Chelsea ambao msimu huu wameyumba walipata goli la kufutia machozi katika dakika ya 65 kupitia Muingereza Chukwunonso Tristan “Noni” Madueke.
Kwa ushindi huo Gunners wanarudi kileleni mwa jedwali la ligi kuu ya Uingereza wakiwa na alama 78 alama 2 mbele ya Man City wenye mechi mbili kiporo.
Chelsea wao wanasalia nafasi ya 12 wakiwa na alama 39 baada ya kucheza mechi 33.
Ligi hiyo aidha inaendelea leo Jumatano sa nne usiku kwa mechi mbili kuchezwa ambapo Liverpool wanawaalika Fulham ugani Anfield huku Man City wakiwa mwenyeji wa West Ham United katika dimba la Etihad.
