Naibu wa rais Rigathi Gachagua sasa anasema atawataja watu anaosema walipora zaidi ya shilingi bilioni 24, miezi mitatu kabla ya mwisho wa utawala wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
Gachagua aliyezungumza eneo la Roysambu jijini Nairobi alidai kuwa hali ngumu ya kiuchumi inashuhudiwa sasa nchini inatokana na uporaji huo, anaodai ulifanyika na baadhi ya mawaziri na makatibu wa serikali ya Kenyatta.
Gachagua amedai kuwa njama ya kuiba fedha za umma ilitekelezwa kati ya tarehe 15 Agosti na tarehe 13 september mwaka jana wakati ambapo kulikuwa na mtafuruku kuhusiana na matokeo ya uchaguzi.
Gachagua ameongeza kuwa muungano wa azimio la umoja one kenya unaoongozwa na Raila Odinga ulinufaika na uongozi ambao anadai ulisababisha na kuchangia pakubwa katika kuzorota kwa hali ya kiuchumi.
Wakati uo huo Gachagua amepinga kuwa serikali ina mpango wa kukandamiza biashara zinazohusishwa na Raila sawia na zile za rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
NAIBU WA RAIS ASEMA ATAWATAJA WALIOPORA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 24

