Himizo linaendelea kutolewa kwa vijana kaunti ya Kilifi na nchini Kote kuzidi kumtumikia mwenyezi Mungu na pia kuhudhuria ibada kanisani ili kuepukana na mambo ambayo, huenda yakawashawishi kupotoka kimaadili.
Akizungumza na Lulu Fm Mchungaji wa kanisa la Life Church International Malindi kaunti ya Kilifi Daniel Nga’ang’a, maarufu kama Danny Gift amesema vijana wengi hawaendi kanisani kutokana na sababu mbalimbali, ambazo zimechangia kwa wengi wao kushawishika na kujihusisha na mambo Maovu, ambayo huwa yanawafanya kuwa mbali na uwepo wa Mungu.
Akizungumzia mkutano wa Injili ambao utaandaliwa kesho Jumamosi na kutamatika siku ya Jumapili katika uwanja wa Alaskan, kwa ushirikiano na kituo hiki cha Lulu Fm na kile cha Pearl Jijini Nairobi, Machungaji Danny Gift amewakaribisha watu wote katika mkutano huo, ambao unalenga kuhubiria watu na kuwajuza umuhimu wa kumjua Mungu na hata kumtumikia ipasavayo kulingana na Biblia.
Mchungaji Danny Gift amesema pia kutakuwa na maombi ya kuliombea taifa la Kenya, ambalo kwa sasa linaendelea kukumbwa na changamoto mbalimbali likiwemo suala la mapenzi ya jinsia moja, ambalo linaendelea kuibua hisia mbalimbali nchini.
Vilevile, amesema Mchungaji Sammy Jeffa wa kanisa la JPCC Malindi ni miongoni mwa wale ambao, watakuwa kwenye mkutano huo wa maombi pamoja na waimbaji mbalimbali wa nyimbo za Injili.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo hiki cha Lulu Fm Janet Kilalo, ameutaja mkutano huo wa maombi kama ambao utakuwa wenye manufaa mengi, Sio kwa Wakristo pekee bali kwa kila mtu na kuhimiza umuhimu wa watu kuhudhuria kwa wingi.
MKUTANO WA MAOMBI KUANDALIWA KESHO KWENYE UWANJA WA ALASKAN MJINI MALINDI
