MBUNGE WA JUJA GEORGE KOIMBURI ATIWA NGUVUNI NA MAAFISA WA DCI.

Maafisa wa usalama wamemtia mbaroni mbunge wa Juja kaunti ya Kiambu, George Koimburi kwa madai ya kusema “serikali kuu, ilitumia shilingi bilioni 13, kumpigia debe Raila Odinga, katika kuwania wadhifa wa mwenyekiti wa tume ya muungano wa taifa ya Afrika AUC”.

Aidha baadhi ya viongozi wanaoegemea upande wa aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagwa, wamejitokeza na kukashifu kitendo hicho, wakisema kuwa usemi wa Koimburi ni sawa kwa mujibu wa sheria, kwani anajukumu la kuchunguza utendakazi wa serikali, kama kiongozi wa bunge la kitaifa.

Wakiongozwa na seneta wa kaunti ya Kiambu, Karungo wa Thang’wa na seneta wa kaunti ya Makueni, Wakili Dan Maanzo wamesema kuwa hatua hiyo, ni ukiukaji wa sheria na ni sababu tosha, za kuwasilishwa kwa mswada wa kumbadua rais William Ruto mamlakani.

Kwa upande wao mawakili wa Koimburi, wakiongozwa na Ndegwa Njiru wamemtetea kiongozi huyo, wakisema alikuwa akitekeleza wajibu wake kama mbunge.