Mahakama ya shanzu imesema kuwa mchungaji Ezekiel Odero wa Kanisa la New Life Prayer Center eneo la Mavueni kaunti ya Kilifi, atasalia korokoroni kwa siku tatu zaidi kupisha uchunguzi dhidi yake, kinyume na matakwa ya idara ya usalama iliyopendekeza kumzuilia kwa siku 30 zaidi.
Hisia mseto zinaendelea kuibuliwa miongoni mwa wakaazi kufuatia kukamatwa kwa mchungaji wa kanisa la New life prayer centre, Ezekiel Odero.
Baadhi ya wakaazi na wafuasi wa mchungaji huyo wamesema kuwa Ezekiel anatuhumiwa bure kwani hajakuwa akihubiri injili potovu kama inavyodaiwa kwenye mashtaka yake.
Badala yake wamesema kuwa amekuwa wa msaada kwa wengi sio tu kiroho lakini pia katika kutoa misaada ya kijamii kwa wenye uhitaji katika jamii.
Hatahivyo wakaazi wengi wamemshutumu vikali, Ezekiel kwa kile walichosema kuwa amekuwa akieneza itikadi potovu akisababisha wengi kutoamini tiba za kisayansi na kuishia kutumia maji yanayodaiwa kuwa ya utakaso sawa na vitambaa.

