Mahakama kuu ya Malindi kaunti ya Kilifi imetupilia mbali kesi iliyowasilishwa katika mahakama hiyo ili kupinga ushindi wa gavana wa kaunti ya Kilifi Gedion Mung’aro ulioandaliwa Agosti tisa mwaka jana wa 2022.
Akitoa uamuzi huo jaji wa mahakama hiyo ya Malindi Anne Onginjo, amesema kesi hiyo ilikosa ushahidi wa kutosha na kusababisha kutupiliwa mbali.
Jaji Onginjo amewaagiza walalamishi wa kesi hiyo kulipa faini ya shilingi milioni sita kwa gavana Mung’aro, naibu wake Florence Chibule na tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC tawi la kaunti ya Kilifi pamoja na afisa mkuu wa tume hiyo kaunti ya Kilifi Hussein Gure.
Kesi hiyo iliwasilishwa na wapiga kura watatu kaunti ya Kilifi ambao ni pamoja na Justice Chinga Chirume, Justin Charo Baya na Salim Chai Tsui, ambao walishtaki tume ya IEBC na gavana Mung’aro Kwa madai uchaguzi huo haukuandaliwa kwa njia ya huru na haki.
Ikumbukwe katika kipute cha uchaguzi mkuu wa Agosti 9 mwaka jana wa 2022, Mungaro ambaye aliwania wadhifa huo wa ugavana akitumia wa chama cha ODM alipata kura 143,773 , Aisha Jumwa wa chama cha UDA 68,894 na George Kithi wa chama cha PAA kupata kura 64,326.
MAHAKAMA YA MALINDI YATUPILIA MBALI KESI ILIYOWASILISHWA KUPINGA USHINDI WA GAVANA MUNG’ARO WA KILIFI

