MAAFISA WANNE WA SSU WANAENDELEA KUZUILIWA KATIKA IDARA YA DCI

Maafisa wanne wa polisi waliokuwa chini ya Kitengo Maalum cha Huduma (SSU), ambacho pia kilivunjiliwa mbali na Rais William Ruto katika afisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), bado wanaendelea kuzuiliwa na polisi katika vituo mbalimbali vya polisi jijini Nairobi wakitarajiwa kufikishwa mahakamani hii leo.
Wanne hao ambao ni pamoja na Inspekta mkuu na makoplo watatu, walikamatwa baada ya kukisiwa kuhusika kwenye tukio la Julai 25 mwaka huu, ambapo raia wawili wenye asili ya Kihindi ambao ni Mohamed Kidwai, Zulfiqar Khan na dereva wao Nicodemus Mwange, walitoweka jijini Nairobi.
Watatu hao walitekwa nyara mnamo Julai 25, 2022.
Haya yanajiri siku chache baada ya mifupa inayoaminika kuwa ya watu waliotekwa nyara, kupatikana katika msitu wa Aberdare baada ya msako wa siku mbili.
Raia hao wa India wanaaminika kualikwa nchini, kusaidia chama cha UDA kwa maandalizi ya uchaguzi, lakini walitoweka katika mazingira yasiyoeleweka.
Zaidi ya maafisa 100 wa polisi walitumwa katika msitu wa Aberdare, kuwatafuta Mohamed Zaid Sami Kidwai, Zulfiqar Ahmad Khan na dereva wao, Nicodemus Mwania Mwange.