KUNA HAJA YA VIJANA NCHINI KUELIMISHWA KUHUSIANA NA BIASHARA.

Kuna haja ya vijana kupewa hamasa kuhusiana na mbinu mbali mbali za kujiendeleza kibiashara, kupitia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya kitaifa katika maeneo yao.

Haya ni kwa mujibu wa shirika la kibiashara la 20x, ambalo limeelezea kuwepo miradi mingi ambayo inaweza kuimarisha shughuli za kibiashara katika jamii.

Akizungumza katika kaunti ya Kwale, kwenye kikao cha kutoa mafunzo ya kibiashara kwa vijana, afisa mkuu mtendaji wa shirika hilo Eunice Maina, amesema kuwa jukumu la serikali ni kuimarisha mazingira ya jamii, kuwa na uwezo wa kufanya biashara za aina mbali mbali ili kujikimu kimaisha.

Eunice amewaonya vijana katika eneo hilo, dhidi ya kuilaumu serikali kwa madai ya kutowasaidia katika kuwaimarisha kibiashara na badala yake kuwa wabunifu katika kutambua aina ya biashara zilizo na uwezo wa kunawiri katika maeneo ambapo serikali, inaendeleza miradi ya maendeleo.

Aidha, baadhi ya vijana waliohudhuria kikao hicho wamesema kuwa ukosefu wa elimu kuhusiana na masuala ya kibiashara, ndiyo chanzo cha wengi wao kutoimarika kiuchumi.