KOGALO YASHINDA FKF – PL, MKUFUNZI WAO AKITANGAZA KUONDOKA

Ushindi wa mabao 3-0 wa klabu ya Gor Mahia inayoongozwa na mkufunzi Journathan Mckinstry  dhidi ya klabu ya Muhoroni Youth jana uliwapa ubingwa wa ligi kuu ya fkf  hapa nchini kwenye msimu huu wa 2023/2024 na wameshinda ubingwa wa ligi hiyo kwa rekodi ya mara 21 sasa .

Magoli katika mechi hiyo yalifungwa na Benson Omala akiingia kambani dakika ya 45, Boniface Omondi akifunga kunako dakika ya 51 na hatimaye Austine Odhiambo akifunga kazi kunako dakika ya 64, mabao hayo yakimsaidia Kogalo kutetea ubingwa wake kwa mara nyingine tena.

Gor Mahia wakiwa na alama 67 wametangazwa mabingwa tayari mechi tatu zikiwa zimesalia msimu huu kutamatika, na hii ni kutokana na utofauti wa alama kwa sasa ikiwa Kogalo wako mbele na alama 11 mbele ya nafasi ya pili Tusker.

Hata hivyo, baada ya mechi mkufunzi mkuu wa klabu hiyo Johnnathan Mckisnrty alitangaza kuwa atakuwa anaachana rasmi na Kogalo na anaenda kuchukua nafasi ya ukufunzi mkuu katika timu ya taifa ya Gambia kipindi hiki cha mashindano ya kuwania tikiti ya kufuzu kwa kombe la dunia.