Mkufunzi wa klabu ya Malindi Clusters Davis Badili amethibitisha kuwa sintofahamu kuhusu uhamisho wa mchezaji wake wa zamani Rafiki Kavoi wameukamilisha na sasa ni rasmi yeye ni mchezaji wa klabu ya Malindi United.
Badili amethibitisha kuwa viongozi wa vilabu wa Malindi Progressive Academy, Malindi United pamoja na Malindi Clusters walikutana wiki ilopita na wakajadili suala hilo na kuafikiana kwa pamoja walipowahusisha viongozi wa FKF katika kaunti ya Kilifi.
Hata hivyo Badili amezikosoa mbinu za usajili wanazotumia Malindi United akisema kwamba wanakosea kwa kukosa uwazi. Kwa kuonyesha kutoridhika na uhamisho huo Badili amedokeza kwamba Rafiki Kavoi atajilaumu mwenyewe iwapo jambo baya litachipuka katika kambi yake mpya akisema kuwa alikosa msimamo.
Rafiki Kavoi alihusishwa pakubwa na uhamisho kuelekea Bandari Youth majuma kadhaa yalopita, uhamisho ambao ulitibuka baada ya kukosa kuachiliwa na Malindi United kwa kile kinachotajwa kuwa bado wako na umuhimu naye kwa sasa.

