KENAFF YAITAKA SERIKALI YA KAUNTI YA KILIFI KUJENGA BWAWA LA KUHIFADHI MAJI

Shirikisho la kitaifa la wakulima nchini (KENAFF) limeitaka serikali ya kaunti ya Kilifi kujenga bwawa la kuhifadhi maji ya mto sabaki, ili yaweze kutumika katika kilimo.
Mwenyekiti wa shirikisho hilo kaunti ya Kilifi Getrude Bahati, anadai maji ya mto huo ni raslimali muhimu inayoweza kutumika kufanikisha kilimo wakati wa ukame iwapo yatahifadhiwa.
Bahati aidha amedokeza kuwa shirikisho hilo linalenga kuishinikiza serikali ya kaunti hii ya kilifi kupitia idara ya kilimo kuwahamasisha wakulima jinsi ya kuhifadhi maji ya mvua.
Mwenyekiti huyo amesisitiza haja ya serikali kuu na zile za kaunti eneo la pwani kuiga mfano wa mbinu za kisasa za kuboresha sekta ya kilimo zinazotumika katika mataifa ya nje.
Hata hivyo Bahati anadai kuwa hatua hiyo itawawezesha wakulima kunufaika na shughuli za kilimo eneo hili na nchi yote kwa jumla.