BAADHI ya wazee kutoka Kaunti ya Kisii wamejitokeza kutangaza kuwa wanaunga mkono azma ya aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Wazee hao, aidha wamedokeza kuwa Dkt Matiang’i atarejea humu nchini hivi karibuni kubuni mikakati zaidi ya kufaulisha azma yake inayolenga kumng’atua mamlakani Rais William Ruto na wakamtaka kiongozi wa chama cha ODM kukoma kumkejeli waziri huyo wa zamani.
Wakiongozwa na aliyekuwa spika wa bunge la kaunti ya Kisii, Bw David Kombo, wazee hao wanaotoka ukoo wa Dkt Matiang’i walitaja mfano wa utendakazi mzuri wa waziri huyo alipokuwa akihudumu katika serikali ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta kama dhihirisho anatosha kuwa rais.
Walisema ufanisi ulioafikiwa na Dkt Matiang’i katika wizara za Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT), Elimu na Masuala ya Ndani ni sababu tosha za kiongozi huyo kupewa jukumu la kuliongoza taifa.
Wazee hao waliwakashifu viongozi kutoka jamii ya Abagusii waliokuwa wakitoa matamshi ya kupuzilia mbali azma ya Dkt Matiang’i wakiunga serikali ya sasa.

