IDADI KUBWA YA VIJANA KAUNTI YA LAMU WAMEATHIRIKA NA UTUMIZI WA DAWA ZA KULEVYA

Gavana wa kaunti ya Lamu Issa Abdalla Timammy ameapa kukabiliana na ulanguzi wa dawa za kulevya kwenye kaunti hiyo.
Timamy amesema idadi kubwa ya vijana katika kaunti hiyo ni waraibu wa dawa za kulevya hali ambayo amesema iwapo hatua thabiti hazitachukuliwa huenda wengi wao wakashindwa kujinasua kwenye utumizi huo.
Amesema wasichana wenye umri mdogo pia wameathirika na utumizi huo na lazima mikakati iwekwe ili maisha yao yasizorote.
Kulingana na Timamy hali ya kusambaratika kwa familia nyingi ni miongoni mwa sababu zinazochangia kwa vijana wengi katika kaunti hiyo kuwa waraibu wa dawa za kulevya.
Aidha, amesema wameanzisha tiba Methadone kwenye hospitali kuu ya King Fahad na kuitaja kuwa yenye manufaa zaidi katika kuwanasua waraibu hao.
Kisiwa cha Amu mtaa wa Wiyoni, Langoni, Kashmiri, faza, Mbwajumwali, Kizingitini, Chundwa, Kisiwa cha Ndhau ni miongoni mwa maeneo ambayo kumekuwa na utumizi mkubwa wa mihadarati