Familia moja eneo la Kasufini, Shella, kaunti ndogo ya Malindi kaunti ya Kilifi inahofia kuwa huenda mwana wao akakosa kutimiza ndoto zake za kujiendeleza kimasomo kutokana na hali ya uchochole unayowakumba.
Wakiongozwa na Mapenzi Katana wanafamilia hao wamesema kuwa hawana uwezo wa kumfikisha msichana wao katika shule ya upili aliyoitwa ya Lirhanda kule kaunti ya Kakamega.
Mapenzi ambaye ni mama ya msichana huyo kwa jina Rita Pili anaugua ugonjwa wa kiharusi na kifua kikuu hali inayofanya ashindwe kumudu gharama za kumuelimisha binti yake mbali na hali ya umaskini inayowakumba kwa sasa.
Kufuatia hilo anaomba wahisani na wafadhili mbalimbali kujitokeza kumsaidia ili aweze kumfikisha mwanawe katika shule ya upili baada ya kumaliza darasa la nane katika shule ya msingi ya Aiport hapa mjini Malindi ambapo alipata jumla ya alama 323.
Mwanafunzi huyo kwa jina Rita Pili anahofia kuwa huenda akashindwa kutimiza ndoto yake ya kuwa daktari iwapo hatamudu kuendeleza masomo yake ya shule ya upili akiwasihi wahisani kujitokeza ili kumsaidia kufanikisha ndoto zake.
Kwa upande wake mchungaji wa kanisa la joyfellowship Zacharia Oketch ambaye pia ni mchungaji wa familia hiyo ametilia pondo swala la uhitaji wa ufadhili wa kimasomo kwa msichana huyo ili aweze kunufaika kama watoto wengine.
FAMILIA YA RITA PILI MWANAFUNZI KUTOKA KASUFINI YAHOFIA HUENDA AKAKOSA KUJIUNGA NA KIDATO CHA KWANZA

