FAMAU MOHAMMED FAMAU AMPONGEZA RAIS WILLIAM SAMOEI RUTO

Mwanaharakati wa kukabiliana na utumizi wa mihadarati kaunti ya Kilifi Famau Mohammed Famau amempongeza Rais William Samoei Ruto kwa kile anachokisema ameimarisha mikakati ya kukabiliana na ulanguzi wa dawa za kulevya eneo la Pwani na taifa la Kenya kwa jumla.
Kulingana na Famau eneo la Pwani, ndilo lililoathirika zaidi na ulanguzi na hata utumizi wa mihadarati na hivyo basi itakuwa afueni kubwa iwapo rais atakabiliana vilivyo na utumizi wa dawa za kulevya kwani vijana wengi wamekuwa waraibu.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari mwanaharakati huyo amesema itakuwa bora zaidi kwa rais Ruto kushirikiana na wakaazi wa eneo la Pwani katika kutatua suala hilo la utumizi wa mihadarati.
Aidha, amemtaka Rais kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya maafisa wa usalama ambao wamekuwa wakishirikiana na walanguzi wa dawa za kulevya katika biashara hiyo haramu.