FAINALI ZA DOLA SUPER CUP KUANDALIWA 21 – 25 AGOSTI 2024

SASA ni rasmi kwamba fainali za michuano ya Dola Super Cup Inter-County zitaandaliwa katika Kaunti ya Mombasa kuanzia Jumatano, 21 Agosti 2024 hadi Jumapili 25 Agosti 2024.

Kwa mujibu wa barua kutoka kwa kamati andalizi kwa timu zilizofaulu kuingia fainali ni kwamba washiriki wote wanatakiwa kuingia kambini huko Mombasa kuanzia Jumanne 20 Agosti 2024 saa kumi jioni.

Barua hiyo imeeleza kuwa fainali hizo zitakuwa na makundi 2 ambapo kila timu itacheza mechi 3 na timu mbili za juu katika kila kundi zitaingia Nusu fainali.

Kamati hiyo andalizi imeunda hatua kuhakikisha mashindano yanaimarika pamoja na vikosi kuwa bora.

Hatua hizo ni pamoja na kuwa kila timu kuruhusiwa kufanya mabadiliko ya wachezaji 3 kutoka eneo la makazi, yaani mahali inapoishi timu.

Kingine ni kuwa kila timu inaruhusiwa kuajiri wachezaji 3 zaidi kutoka timu yoyote ndani ya Kaunti husika. Wachezaji hao 3 lazima wawe wamecheza wakati wa mchujo.

Kamati hiyo iliongeza kuwa kila timu lazima iwe na kikosi cha wachezaji 23 na viongozi 5 ambao watahudumiwa na Dola Group Of Companies.