Talanta miongoni mwa wakaazi hususan vijana katika kaunti ya Kilifi huenda zikaimarika zaidi baada ya serikali ya kaunti hii kwa ushirikiano na shirika la World Talent Federation kuafikiana kujenga chuo kikuu cha kukuza talanata katika eneo la mariakani.
Kulingana na gavana wa kaunti ya kilifi Gideon Maitha Mung’aro, ni kuwa shirika hilo litawekeza takriban shillingi billioni 10 katika mradi huo.
Mung’aro amesema tayari wamepata ekari 300 zitakazowekezwa mradi huo ambao ameutaja kama moja ya utakaobadilisha maisha ya vijana wengi Kaunti ya Kilifi baada ya kukamilika.
Akizungumza afisini mwake baada ya kukutana na wafadhili wa shirika hilo wakiongozwa na Steve Smith na Alexander Niklasch, gavana Mungaro amebainisha kwamba wawekezaji hao walikuwa na vigezo tofauti walivyoweka ikiwemo miundo msingi bora ya Barabara ambapo eneo la Mariakani lilionekana bora Zaidi.
Mung`aro hata hivyo amesisitiza kwamba chuo hicho kitakuza talanta mbali mbali ikiwemo michezo,Sanaa na uchoraji.

