BUMBANI STARS YAIMARISHWA NA MECHI KUBWA ZA KIRAFIKI

Mkufunzi wa klabu ya Bumbani Stars kutoka kaunti ya Kwale Mwaduka Bakari anasema kushiriki mechi za kirafiki na vilabu vikubwa kama vile Coastal Union ya Tanzania Bara ni kati ya siri ya mafanikio ya timu yake msimu huu.

Bumbani Stars ambao wanacheza msimu wao wa kwanza wa daraja la pili kitaifa wanaongoza ligi na lengo lao kubwa ni kupanda daraja la kwanza.

Mwaduka akizungumza na Tama La Spoti anasema mechi za kirafiki na timu kubwa kumewasaidia kujijenga vilivyo na kuona rahisi kumenyana na wapinzani wao hasa mkoa huu wa Pwani katika ligi.

Ameeleza kuwa msimu huu walipanga kupiga mechi ya kirafiki na klabu ya Simba SC kutoka Tanzania ambayoilitibuka kutokana na wapinzani wao kuwa katika msimu wa Ramadhani.

Amesema kwamba kama klabu wanapanga kuandaa ratiba mpya ya mechi za kirafiki na vilabu vikubwa ili kujiimarisha zaidi lakini pia kufanya wachezaji wake wazidi kupata uzoefu.