BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI LAAPISHWA

Baraza jipya la mawaziri 22 nchini Kenya limeapishwa rasmi leo baada ya kuidhibishwa jana bungeni.
Rais William Samoei Ruto amebakia na waziri mmoja kutoka katika baraza la mawaziri la mtangulizi wake kama mshauri wa masuala ya usalama na kuanzisha wadhifa wa Waziri mkuu ambao haukuwepo kwenye baraza la mawaziri lililopita.
Gavana wa zamani wa benki kuu, Njuguna Ndung’u, sasa ndiye Waziri wa fedha, huku spika wa zamani, Justin Muturi, akiwa mwanasheria mkuu.
Akizungumza baada ya shughuli ya kuwaapisha mawaziri hao, rais Ruto amewataka mawaziri hao kufanikisha ajenda za serikali ya Kenya kwanza huku jukumu la moja kwa moja la baraza hilo jipya la mawaziri litakuwa ni kupunguza gharama ya maisha na mzozo wa chakula uliosababishwa na ukosefu wa mvua.
Rais Ruto amewataka mawaziri hao kuzuru nyanjani kuhakikisha kuwa wanatambua changamoto zinazowakumba wakenya na kubuni njia mwafaka za kutatua na kukabiliana na changamoto hizo.