Mwenyekiti wa kamati ya maji, Raslimali, utalii na Mazingira katika baraza la magavana nchini ambaye pia ni gavana wa kaunti ya Taita Taveta Andrew Mwadime amesema wameafikiana na wizara ya maji kubuni jopo ambalo litafanyia marekebisho ya sheria inayosimamia raslimali za maji mwaka 2016.
Mwadime amesema hatua hiyo inalenga kuweka wazi majukumu ya serikali kuu na zile za kaunti kuhusu suala la usambazaji maji kwa wananchi walioko mashinani.
Jopo kazi hilo limepewa hadi miezi 6 ijayo kuunda ripoti yake na kuwasilisha mapendekezo hayo kwa kamati hiyo na wizara ya maji nchini.
Mwadime ambaye alikuwa akizungumza kwenye kaunti ya Mombasa baada ya kikao na waziri wa maji nchini Alice Wahome, amesema wameafikiana kuhimiza ushirikiano kati ya serikali na sekta ya kibinafsi katika kufanikisha mpango wa serikali wa kujenga jumla ya mabwawa 100 maeneo mbalimbali nchini kama njia moja ya kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa na pia kuimarisha sekta ya Kilimo.
Aidha, amesema wataboresha mipangilio na raslimali za maji kwenye kaunti ili kuimarisha shughuli za usambazaji maji kwa mwananchi.
ANDREW MWADIME ASEMA WAMEAFIKIANA NA WIZARA YA MAJI NCHINI KUBUNI JOPO LAKUFANYIA MAREKEBISHO YA SHERIA

