Niafueni kwa wakaazi wa kaunti ya Lamu wanaokabiliwa na changamoto za kutafuta huduma za afisi ya mkuu wa sheria nchini baada ya afisi hiyo kufunguliwa rasmi katika kaunti hiyo.
Akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi rasmi wa afisi hiyo, mwanasheria mkuu Shedrack Mose amesema kuwa wananchi wa kaunti ya Lamu sasa watapata fursa ya kufahamu masuala mengi zaidi kuhusiana na sheria za taifa.
Mose ambaye alimuwakilisha mwanasheria mkuu nchini Dorcas Oduor amewataka wananchi wa Lamu sasa kuwasilisha malalamishi yao ya kukosa haki dhidi ya masuala mbali mbali kwenye afisi hiyo.
Kauli yake imeungwa mkono na hakimu wa mahakama ya Lamu, Flavian Mulama ambaye amesema kuwa awali wanajamii wa kaunti hiyo, walilazimika kusafiri hadi Mjini Malindi kaunti ya Kilifi ama hata Mombasa ili kupata huduma muhimu za afisi hiyo.

