Timu ya taifa ya Morocco imebanduliwa nje ya michuano ya AFCON kwa kukubali kipigo cha magoli 2-0 walichopokezwa na Afrika kusini katika hatua ya 16 bora ya michuano hiyo inayoendelea Côte d’Ivoire.
Goli la fowadi kinda mwenye umri wa miaka 23 Evidence Makgopa ambaye ni sajili wa Orlando Pirates liliwapa Afrika Kusini uongozi wa mechi hiyo baada ya kutoka sare tasa kwenye kipindi cha kwanza cha mechi hiyo.
Dakika nne za za nyongeza katika kipindi cha lala salama zilimwona beki wa klabu ya Manchester United Sofyan Amrabat akipewa nyekundu na kuifanya Morocco kuumaliza mchezo wakiwa bila huduma zake.
Dakika moja baada ya tukio hilo Afrika kusini kupitia Teboho Makoena wakaongeza goli la pili na la mwisho kwenye mchezo huo.
Kwa ushindi huo Afrika kusini wamefuzu kuingia hatua ya robo fainali na watamenya na Cape Verde waliofuzu kwa ushindi wa goli moja kwa sifuri dhidi ya Mauritania.
Morocco wao wataendelea kutafuta kuzima kiu yao ya kunyakua ubingwa wa kombe la AFCON kwa mara ya pili katika kipute cha AFCON cha 2027 kinachotarajiwa kuandaliwa Afrika Mashariki.
Mara ya mwisho Morocco kushinda AFCON ilikuwa 1976.
Hakuna Senegal wala Sadio Mane, hakuna Morocco, Misri nje, hakuna Ghana, wala Cameroon, Algeria wamekuwa mashabiki yaani wao pia wamerudi nyumabni hawamo mashindanoni, hakuna Tunisia.
Nigeria, mwenyeji Ivory Coast, Cape Verde zimefuzu kwa robo fainali na sasa Afrika Kusini. AFCON mara hii imeonesha maajabu timu zilizoonekana ndogo zikibandua wababe.
Ila je, Cape Verde, Angola, Guinea au DR Congo wanaweza kuandika majina yao katika historia ya Ubingwa kwenye AFCON 2023?

