Ni afueni kwa Wahudumu wa afya ambao waliajiriwa ili kufanikisha mpango wa afya kwa wote UHC, baada serikali kuu kutangaza kuwa sasa itawaajiri kwa mkataba wa kudumu, na ulio na malipo ya uzeeni yaani permanent and pensionable.
Wahudumu hao zaidi ya elfu saba, waliajiriwa kwa kandarasi za muda wa mwaka, mnamo mwaka wa 2019 huku wakaahidiwa Kandarasi za kudumu, baada ya miaka mitatu, lakini hilo halijafanyika hadi leo.
Baada ya kile kimetajwa kuwa mashauriano ya kina, waziri Duale amesema wote wataajiriwa kwenye kandarasi za kudumu, kuanzia tarehe moja mwezi Septemba, ambayo ni Jumatatu ijayo.
Tangazo lake ni tofauti na msimamo wake wa awali, kwamba serikali haina pesa za kuwaajiri wahudumu hao.
Hata hivyo Duale amesema kuna wale ambao wanakabiliwa na kesi kuhusu utovu wa nidhamu, watasubiri kwa muda kabla ya kujua hatma yao.
Wahudumu hao wamekuwa kwenye migomo na maandamano ya mara kwa mara, wakishinikiza kuajiriwa na kupewa kandarasi ya kudumu.
Mapema mwaka huu, waziri wa afya Aden Duale alitangaza kuwa watahamishiwa kutoka kwa serikali ya kitaifa na kuwakabidhi kwa serikali za kaunti, ili magavana washughulikie mishahara yao, pendekezo ambalo limepingwa vikali na viongozi wa Kaunti, pamoja na wauguzi wa UHC.
Wauguzi hao wamesisitiza kuwa waliajiriwa na serikali kuu na mpango wa afya kwa wote UHC ni mpango ulioanzishwa na serikali kuu.

