MAAFISA WA AFYA NYANJANI KAUNTI YA KILIFI WALALAMIKIA KUCHELEWESHWA KWA MALIPO YAO.

Takriban wahudumu 4,000 wa afya ya nyanjani (CHP) kaunti ya Kilifi wanalalamikia serikali ya kaunti kucheleweshwa malipo yao, kwa takriban miezi 6 sasa.

Mwenyekiti wa wahudumu hao John Charo, anasema kuwa serikali ya kaunti iliwalipa kwa kipindi cha miezi 3 pekee, licha ya kutoa ahadi ya kuwalipa maafisa hao wa nyanjani, ili kufanikisha mpango wa utoaji huduma za afya mashinani.

Charo aidha amedokeza kuwa hali hiyo, imekuwa changamoto kwao katika utekelezaji wa shughuli zao na kuathiri afya ya jamii mashinani.

Wakati huo huo mwenyekiti huyo ameelezea kusikitishwa na hatua ya serikali ya kaunti, kutowajumuisha katika malipo ya bima ya SHA, licha ya wao kuendeleza usajili wa bima hiyo kwa jamii.