Timu ya taifa ya kinadada ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 18 Junior Starlets imesalia na kiunzi kimoja pekee wacheze mashindano ya kombe la dunia mwaka huu kwa wachezaji wachanga.
Hii ni baada ya jana kusajili ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Burundi huko Addis Ababa Ethiopia ambako mabao ya Lorna Faith, Marion Serenge, Susan Akoth ndio yaliwapa ushindi huo.
Kulingana na kocha wao Ann Aluoch ni kuwa uzoefu wa kucheza katika uwanja huo ndio jambo ambalo liliwawezesha kusajili ushindi na kuzidisha matumaini yao ya kuwa kikosi cha kwanza cha soka hapa nchini kuwahi kucheza mashindano ya kombe la dunia.
Timu hiyo imewasili leo kutoka Ethiopia na imepokelewa kishujaa katika uwanja wa ndege wa JKIA huku waziri Namwamba akiwa kati ya viongozi mashuhuri walioipokea timu hiyo.

