Changamoto za kifedha ndio jambo ambalo limechangia vilabu vingi vya pwani vinavyoshiriki ligi ya daraja la kwanza kushuka kiviwango msimu huu. Hiyo ni kulingana na msemaji lakini pia katibu mkuu wa Vilabu vya Malindi United lakini pia Malindi Progressive Academy Alex Jumba.
Kulingana na Alex ni kuwa vilabu vya Pwani kama vile Young Bulls na Malindi Unitedkutoka mkoa huu wa Pwani vimeteremka sana kwa kukosa ufadhili wa kutosha kifedha, jambo ambalo limefanya baadhi ya wachezaji kucheza bila motisha ikilinganisha na wachezaji kutoka vilabu vya kaunti nyingine kama vile Nairobi.
”Vilabu vingi huku kwetu vinalemewa na ufadhili. Unapata mwekezaji mmoja anashikilia timu msimu mzima na hata yeye hulemewa. Kusafiri kutoka Pwani mpaka Nairobi ni kipengele wajua kwa hivyo viwango vya wachezaji hushuka kutokana na kukosa malipo, malipo ambayo pia ni motisha kwao.” Alisema Jumba.
Alex amethibitisha rasmi kuwa klabu ya Malindi United zamani ikijulikana kama Malindi Progressive Academy, klabu ambayo inamilikiwa na mwakilishi wadi wa wadi ya Malindi mjini Rashid Odhiambo imeshuka daraja kutoka ligi ya daraja la kwanza hadi daraja la pili kutokana na viwango vyao msimu huu.
”Kwa sasa natibithisha kwa umma kuwa ni kweli tumeshuka. Hii ni kutokana na msimamo wetu katika ligi. Hata tumeazimia kuachana na ratiba za mwisho wa msimu.” Aliongeza Alex

