RASHID ABDALLA SUPER CUP KUNGÓA NANGA KIBINGWA, TIMU 32 KUSHIRIKI

Kipute cha RASHID ABDALLA SUPER CUP chatazamiwa kurindimwa kwa mfumo wa kipekee tofauti na mfumo uliotumiwa katika awamu za awali za michuano hiyo.

Akiongea na TAMA LA SPOTI Kaka Zema, ambaye ni mmoja wa wanakamati wanaoandaa ligi hiyo, amesema kwamba toleo hili la nne litachezwa kutumia mfumo wa mashindano ya Klabu Binwa bara Ulaya.

“Makala ya tatu tulikuwa na vitengo viwili. Tulikuwa na Main Category na Open Category ambapo kwa Main tulikuwa tunazungumzia kile kitengo cha timu ambazo zinatoka sehemu ya Wara Ngómbeni halafu kuna Open Category cha timu ambazo zinatoka katika sub-counties nyengine katika kaunti ya Kwale.

“Lakini ukiangalia utofauti ambao unakuja hapo tayari moja kwa moja katika makala ya nne tumesema kwamba twende kiKombe la dunia, twende kiChampions League wale ambao watakuwa wanaelewa. Timu 32 lakini anatafiutwa mtu mmoja.

“Tumevunja ile main na open categories tukazileta pamoja timu zote katika kaunti ya Kwale. Na mara hii tunasema kwamba ukishatoka kwenye makundi, kuna raundi ya kumi na sita (16), kuna robo fainali na nusu fainali kisha fainali yenyewe. Kwa hiyo kuna utofauti,”amesema Zema.

Zema amedokeza kwamba kipute hicho kinalenga kuboresha thamani ya mchezo wa soka, kutoa ajira kwa vijana lakini pia kuwaleta viongozi pamoja.

“Malengo ya Rashidi Abdalla Super Cup ni kuhamasisha vijana kutojihusisha na uhalifu, kutojihusha na maswala mazima ya dawa za kulevya, kuthamini michezo kwa sababu ukiangalia vilevile katika mtaala wa elimu sasa hivi maswala ya michezo yamepewa kipaumbele sana.

“Kwa mantiki hiyo tumekuja na mashindano haya kuona vipaji vya hawa vijana ambao wanachipuka wanainuka ili pia na wao waweze kuona kwamba wana nafasi ya kuweza kusonga mbele unapozungumzia mchezo wa soka.

“Pia tunalenga kuileta kaunti yetu ya Kwale pamoja si tu kwa wachezaji ama mashabiki lakini pia viongozi. Mfano tu kwenye makala iliyopita kuna viongozi ambao walikuwa wanashindania nyadhfa mbali mbali lakini wakati wa fainali tuliwaleta jukwaa moja na zaidi ya hayo tunatengeneza nafasi za ajira,” amesema Zema.

Zema ambaye pia ni mwanahabari nguli wa michezo chini amesema kwamba kama viongozi wa kipute hicho wanamaono ya kupanua mipaka yao na kuyafanya mashindano hayo kuwa na sura ya kitaifa na kushirikisha timu kutoka kila pembe ya nchi ya Kenya.

Rashid Abdalla Super Cup inatazamiwa kuanza Jumapili Agosti 13 2023 katika uwanja wa shule ya msingi ya Waa. Bingwa mtetezi wa michuano hiyo Denmark FC itamenyana na Kwale United katika mechi ya ufunguzi.