Mkufunzi wa klabu ya Malindi Progressive Bill Mwangemi anasema kwamba ako na matumaini makubwa kuwa klabu yake bado iko na nafasi ya kufuzu kupanda daraja na kushiriki katika ligi ya National Super League msimu ujao.
Kulingana na mwangemi ni kwamba licha ya changamoto ya kukosa muendelezo wa matokeo bora msimu huu hasa baada ya wachezaji nyota kuondoka katika kikosi cha Malindi Progressive, bado nafasi wanayo ya kutetea nafasi ya kupanda daraja.
”Bado nafasi ya kupanda iko, mechi bado hazijaisha na pengo sio kubwa sana. Tumekuwa na changamoto mechi kadhaa lakini hatujavunjika moyo manake hayo ndiyo ya soka.” Alisema Bill
Hata hivyo Mwangemi amesema kwamba licha ya kuwepo na uhasama mkubwa kati yao na mahasimu wao Young Bulls katika ligi hiyo, Young Bulls kulingana na kiwango chao msimu huu wanastahili kupanda hadi National Super League.
”Kwa msimu huu kusema ukweli Young Bulls wamekuwa na msimu mzuri. Bila kuegemea upande wowote nitasema, iwapo watapanda hadi National Super League basi tutazidi kujivunia kama wakazi wa Malindi manake timu zote ni zetu hizi. Pia sisi tunajikaza tupande. Hatujakata tamaa bado mechi ziko” Alisema Bill.

