TUNAOMBA UFADHILI – BEACH BAY

Mweka hazina wa klabu ya Beach Bay Clara Kadzo ameomba wahisani kufadhili klabu yake ili kuifanya klabu hiyo kuwa na mafanikio na kuandikisha historia ya kupanda daraja hadi daraja la kwanza kitaifa.

Klabu hiyo imekuwa ikiyumba hasa katika msimu huu kutokana na ukata wa kifedha jambo ambalo limekuwa likifanya klabu hiyo kukosa kuheshimu ratiba mara kadhaa msimu huu.

Clara ametoa wito kwa wahisani kujitokeza kufadhili klabu hiyo akiwa na imani kwamba klabu yake inauwezo mkubwa wa kuleta mafanikio.

”Mimi nakwambia ukweli, hii timu yangu ya Beach Bay ninavyoiona ingekuwa si mambo ya ukosefu wa pesa saa hii ingekuwa mbali sana. Mimi naomba hata kama ni mfadhili atakuja kwetu na masharti atupe udhamini mwaka mmoja tusipopanda daraja atuachilie, nina uhakika tutapanda. Kwa sasa tukotuko tu wakati mwengine mechi yaeza kuwa ni kesho na mpaka sasa hatutajua kama tutasafiri au la!” Alisema Clara.

”Tarehe 27 mwezi Mei ambayo ni wikendi hii tunapanga tufanye mchango tuone tutafikia wapi, kwa sababu tarehe 28 Mei tuko na mechi na Simba Apparel na hatutajuwa kama tutasafiri au vipi. Kwa hivyo huo mchango ni muhimu sana.” Clara aliongeza

Wikendi ijayo Beach Bay inalenga kufanya mchango ili kuipiga jeki klabu hiyo angalau kumaliza msimu vizuri na kuepuka kushuka daraja.