JAMII YAONYWA DHIDI YA KUWASHUTUMU WAUMINI WA DINI YA KIKRISTO.

Mkewe naibu rais Rigathi Gachagua, Kasisi Dorcas Gachagua amesema kuwa makanisa na wakristo hawapaswi kukemewa kwa jumla kutokana na makosa ya viongozi wachache waliojitambulisha kuwa wachungaji.

Mkewe naibu rais ameyasema haya akiikashifu itikadi potovu inayoendelezwa na mchungaji mwenye utata, Paul Mackenzie akimtaja kuwa mhalifu hukua akisisitiza kuwa makosa ya Mackenzie yasilimbikiziwe wachungaji wote wala kanisa kwa jumla.

Kasisi Dorcas akizungumza katika hafla ya kuwapa wajane chakula jijini Nairobi, amesema kuwa sio sahihi kwa makanisa yote kulaumiwa kutokana na makosa ya Mackenzie huku akisema kuwa hata familia yake haipaswi kuingizwa kwenye utata unaomgubika Mackenzie.

Naye naibu rais Rigathi Gachagua akizungumza kwenye hafla tofauti jijini Nairobi ametetea kanisa akionyesha kuunga mkono kauli ya mkewe akishinikiza wananchi wakome kukashifu kanisa kwa jumla kwa sababu ya makosa ya viongozi wachache wa kidini.