YANGA YAUGULIA MAAFA YA WACHEZAJI WAO

Mkufunzi Collins Omol anasema kwamba klabu yake ya Yanga FC inayoshiriki ligi ya daraja la pili kitaifa inakabiliwa na kipindi kigumu kurudisha motisha miongoni mwa wachezaji baada ya wachezaji watatu wa timu hiyo kufariki dunia kutokana na ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha basi la chuo kikuu cha pwani walilokuwa wameabiri kuelekea michezoni katika kaunti ya Nakuru tarehe 30 mwezi Machi.

Omol amesema kwamba kwa sasa wanajitayarisha kwa mazishi ya wachezaji hao na amesema kwa sasa wanalenga kuleta washauri kwa wachezaji wake ambao bado wametaharuki kutokana na ajali hiyo mbaya akisema baadhi ya wachezaji wamekuwa wakisusia kusafiri kwa mechi kutokana na hofu baada ya tukio lililogharibu wachezaji wenzao.

Kesho Yanga FC watakuwa wanavaana na Beach Bay mwendo wa saa tisa mchana katika uwanja wa Mjanaheri eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi.