MCHUNGAJI PAUL MACKENZIE AACHILIWA KWA DHAMANA

Mchungaji wa kanisa la Good News international kaunti ya Kilifi Paul Mackenzie amefikishwa katika mahakama ya Malindi kaunti ya Kilifi kwa madai ya kuhusika kwenye visa vya mauaji ya watoto wawili.
Akiwa mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Olga Onalo mahakama imearifiwa mnamo tarehe 16 na 17 mwezi wa tatu mwaka 2023 mshukiwa huyo anadaiwa kusababisha vifo vya watoto wawili baada ya kuwashawishi kufunga ambapo walikosa kula chakula na kuaga dunia na kisha miili yao kuzikwa katika eneo la Chakama.
Afisa wa Upelelezi wa makosa ya jinai DCI, anayechunguza kesi hiyo Joseph Yator ameambia mahakama hiyo ya Malindi kuwa mhubiri huyo alikamatwa baada ya kuhusika kwa vifo vya watoto hao.
Hatahivyo ombi la afisa huyo wa Upelelezi wa jinai kutaka mahakama kuamuru mchungaji Mackenzie azuiliwe kwa mda wa siku 15 limekataliwa.
Wakili wa Mackenzie, Elisha Komora amesema ripoti kutoka kwa maafisa wa Upelelezi wa jinai haijaelezea ni wapi mhubiri huyo alihusika kwenye mauji ya watoto hao.
Hakimu wa mahakama hiyo ameamuru kuachiliwa kwa Paul Mackenzie kwa dhamana ya shilingi elfu 10,000 huku akiamuru mhubiri huyo kujiwasilisha katika kituo cha polisi cha malindi iwapo atahitajika.