Baadhi ya Viongozi wa dini ya kiislamu eneo bunge la Malindi kaunti ya Kilifi wametoa wito kwa Wakenya, kujitokeza na kupinga mapenzi ya watu wa jinsia moja kuoana.
Wakiongozwa na aliyekuwa mwenyekiti wa Malindi Supreme Council Sheik Salim Omar Juma, ametaja mapenzi hayo kuwa kinyume cha maadili ya dini hiyo na kusema Mungu hulaani kila taifa linalohalalisha mapenzi ya jinsia moja.
Akizungumza katika kikao na wanahabari mjini Malindi kaunti ya Kilifi, kiongozi huyo amenyooshea kidole cha lawama mataifa yanayounga mkono ushoga na usagaji ulimwenguni, kwa madai ya kushawishi taifa la Kenya kujihusisha na suala hilo, ili kusaidiwa kukabiliana na hali ngumu ya ukame na baa la njaa nchini.
Aidha, Sheik Juma amemuonya jaji kuu nchini Martha Koome, dhidi ya kuhalalisha ushoga na usagaji nchini huku kauli yake ikiungwa mkono na Ustadh Salim Tadhfaza, ambaye amesema wataungana na waumini wa dini ya kikristo, ili kufanya maombi ya kupinga suala hilo na hata kumuomba Mungu kuwaondolea suala hilo katika jamii.
SUALA LA USHOGA NA USAGAJI LAZIDI KUIBUA HISIA MSETO MIONGONI MWA VIONGOZI WA DINI YA KIISLAMU MALINDI

