Gavana wa kaunti ya Kilifi Gedion Maitha Mung’aro amesema magavana wote wa kaunti za pwani wataungana na kisha kuwasilisha matakwa yao kwa rais William Samoei Ruto.
Akizungumza kwenye kaunti ya Mombasa katika kongamano la Muungano wa Jumuiya ya kaunti za pwani na mawaziri wa fedha kutoka ukanda wa pwani, Mung’aro ambaye pia ni mwenyekiti wa muungano huo amesema miongoni mwa matakwa yao ni ile ya ulipaji Fidia kwa wavuvi wa Pwani hasa wale ambao waliathirika na ujenzi wa mradi wa bandari ya Lapsset kaunti ya Lamu.
Mung’aro amesema hata baada ya shughuli za uvuvi kuathirika na bandari hiyo, wavuvi katika kaunti ya Lamu wanaendelea kuhangaika wakiendelea kusubiri fidia yao ya shilingi bilioni 3.7.
Aidha, Gavana Mung’aro ametaka Bunge la kitaifa na Lile la seneti kupitisha sheria ya uvuvi ili kuboresha sekta ya uvuvi kanda ya pwani.
MAGAVANA WA PWANI KUWASILISHA MATAKWA YAO KWA RAIS WILLIAM SAMOEI RUTO

